Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban na Mkuu wa Red Cross watoa wito wa kumaliza mateso

Ban na Mkuu wa Red Cross watoa wito wa kumaliza mateso

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Rais wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, Peter Maurer, wametoia onyo la pamoja kuhusu athari za mizozo iliyopo sasa dhidi ya raia, na kutoa wito hatua madhubuti za dharura zichukuliwe ili kushughulikia mateso kwa binadamu na kutokuwepo usalama.

Viongozi hao wawili wamesisitiza umuhimu wa kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ili kumaliza machafuko na kuzuia mivutano zaidi.

Kwa mantiki hiyo, wametoa wito kwa serikali ziongeze juhudi za kutafuta masuluhu endelevu kwa mizozo.

Aidha, wamezitaka serikali zitumie ushawishi wao binafsi au kwa pamoja dhidi ya pande zilizoko kwenye mizozo ya silaha ziheshimu sheria, ikiwemo kufanya uchunguzi wa kina katika uvunjaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, kuwawajibisha wahalifu na kuweka mikakati ya kuhakikisha sheria inaheshimika.

Wamezitaka serikali pia ziwalaani wote wanaofanya ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, mathalan mashambulizi ya kukusudia dhidi ya raia na miundo mbinu ya kiraia.

Viongozi hao pia wamezitaka seriklali zihakikishe raia wanafikiwa na wahudumu wa afya na kibinadamu , pamoja na kuwalinda wahudumu wa afya na wa kibinadamu.