Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalam wa UM ataka haki ya elimu ilindwe katika ubia wa sekta binafsi na ya umma

Mtaalam wa UM ataka haki ya elimu ilindwe katika ubia wa sekta binafsi na ya umma

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya kupata elimu, Kishore Singh, ametoa wito kwa nchi zote wanachama wa Umoja huo kuangazia uimarishaji wa haki ya kupata elimu wakati zikisaka ubia katika utoaji elimu.

Mtaalam huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuheshimu haki za binadamu ni muhimu hata zaidi wakati wa kusaini mikataba ya kuwezesha utimizaji wa haki kama vile ya kupata elimu.

Ameweka msisitizo kwa majukumu ya serikali katika kulinda maslahi ya umma wakati zinaposaini mikataba ya ubia na wadau wengine. Ameelezea wasiwasi wake kuhusu hatari nyingi zinazotokana na ubia na sekta binafsi, na kutaja wajibu wa serikali wa kuweka sheria na utaratibu mwafaka, pamoja na vigezo vya kufuatilia na kupunguza hatari ya ubia huo kutumika vibaya.

Amehimiza serikali zitafute wadau wanaojali maslahi ya jamii na wenye moyo wa ukarimu, na kukataa kauli kuwa bila faida, hakuna mtoa huduma za elimu binafsi atataka kufungua shule.