Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laahidi kuendelea kufanya mijadala ya wazi

Baraza la Usalama laahidi kuendelea kufanya mijadala ya wazi

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limekaribisha kuendelea kushiriki kwa wajumbe zaidi katika mjadala wake wa wazi wa Oktoba 20, 2015 kuhusu utekelezaji wa taarifa ya rais wake namba S/2010/507.

Katika taarifa ya rais wake, Baraza hilo limeeleza nia yake ya kuendelea kufanya mjadala wa kila mwaka kuhusu utendaji kazi wake, na kuahidi kuendelea kutathmini mbinu zake za utendaji kazi ili kuhakikisha kuwa zinafaa na zinatekelezwa ipasavyo.

Aidha Baraza la Usalama limekumbusha kuhusu ahadi yake ya kutumia mara kwa mara mijadala ya wazi, na hivyo kukaribisha taarifa za pamoja zinazotolewa na wanachama wake na nchi zingine wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Halikadhalika, Baraza la Usalama limesisitiza umuhimu wa kuongeza uratibu, ushirikiano na uhusiano na vyombo vingine vikuu vya Umoja wa Mataifa, hususan Baraza Kuu, Baraza la Kiuchumi na Kijamii , Sekritarieti, pamoja na vyombo vingine kama Kamisheni ya Ujenzi wa Amani na mashirika ya kikanda kama Muungano wa Afrika, AU.