Ghasia yazuia masomo kwa mamilioni ya watoto nchini Iraq

30 Oktoba 2015

Takribani watoto Milioni Mbili hawako shuleni nchini Iraq, na wengine zaidi ya Milioni Moja wako hatarini kuacha shule kwa sababu ya mzozo na vurugu nchini humo.

Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF likisema kwamba tatizo hilo linawakumba zaidi watoto wa wakimbizi wa Syria na wale waliolazimika kuhama makwao.

Kwenye taarifa hiyo Mwakilishi wa UNICEF nchini Iraq Peter Hawkins amenukuliwa akisema kwamba Iraq iko hatarini kupoteza kizazi kizima.

Aidha UNICEF imeeleza kwamba karibu shule moja kati ya tano haiwezi kutumiwa kwa ajili ya masomo kwa sababu imeteketezwa, kuharibiwa au kutumiwa na jeshi au wakimbizi.

Vile vile mwaka 2014 mashambulizi 67 yameripotiwa dhidi ya shule au walimu.

Hata hivyo UNICEF imesma mwaka 2014, imejenga shule mpya 40 na kutengeneza zaidi ya maeneo ya muda 1,500 kwa ajili ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud