Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kampeni ya chanjo dhidi ya kipindupindu kuanza Iraq

Kampeni ya chanjo dhidi ya kipindupindu kuanza Iraq

Shirika la Afya Duniani WHO limejiandaa kuzindua kampeni ya chanjo dhidi ya kipindupindu ili kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo ulioanza tarehe 15 Septemba nchini Iraq.

Tayari dozi zaidi ya 500,000 zimeandaliwa nchini humo, na hiyo ni kwa mujibu wa msemaji wa WHO huko Geneva, Uswisi, Fadela Chaib alipozungumza na waandishi wa habari.

Ameeleza kwamba kuzidi kuzorota kwa hali ya usalama, idadi kubwa ya watu kukimbia makwao pamoja na kusambaratika kwa huduma za afya vinazidi kuchochea hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo.

Tayari idadi ya visa imefikia zaidi ya 2,000, na hadi sasa hata hivyo hakuna hata mtu mmoja aliyefariki dunia kwa sababu ya kipindupundu.

Hata hivyo Bi Chaib ameeleza kwamba chanjo haitoshi :

“Kutoa maji safi na salama, huduma za vyoo na usafi ni msingi katika kuzuia na kudhibiti kipindupindu. Chanjo ya kipindupindu ni nyenzo salama ya ziada yenye ufanisi ambayo inaweza kutumiwa kando mwa harakati zingine za kudhibiti kipindupindu, na siyo kuchukua nafasi zake.¨