Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DPI imetoa taarifa sahihi kwa jumuiya ya kimataifa : Gallach

DPI imetoa taarifa sahihi kwa jumuiya ya kimataifa : Gallach

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Idara ya taarifa kwa umma DPI, Bi Cristina Gallach amesema idara yake  imefanya kazi kubwa katika kuufahimsha umma mambo mengi ya Umoja wa Mataifa hususani wakati wa maadhimisho ya maika 70 ya umoja huo.

Akihutubia kamati maalum ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kuondokana na ukoloni, Bi Gallach amesema kimsingi DPI ina wajibu wa kufahamisha jamii kwa ufasaha pasi na upendeleo wowote na kwa wakati na urari, kuhusu majukumu ya Umoja wa Mataifa ili kukuza msaada wa jumuiya ya kimataifa kwa kazi za umoja huo na kwa uwazi mkubwa.

Amesema DPI imetumia vyema mwanya wa mkutano wa baraza la kuu la Umoja wa Mataifa uliowaleta pamoja wakuu wa nchi wanachama kujulisha jumuiya ya kimataifa kuhusu jukumu la kipekee na vipaumbele katika kufikia suluhisho katika changamoto za pamoja.

Kuhusu kutumia mitandao ya kijamii, mkuu huyo wa DPI amesema kumewezesha kufika katika maeneo ambayo majukwaa asilia hayafiki akitolea mfano wa idhaa ya Kichina ambayo imepata watazamaji milioni 130 na zaidi ya maoni 63,000 kutoka kwa jamii.