Hali ya kibinadamu Sudan, Sudan Kusini na Somalia bado ni tete- OCHA

Hali ya kibinadamu Sudan, Sudan Kusini na Somalia bado ni tete- OCHA

Mkuu wa Operesheni za Kibinadamu katika Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibidamu, OCHA, John Ging, amesema kuwa hali ya kibinadamu katika nchi za Sudan, Sudan Kusini na Somalia ni mbaya sana, kwa kuzingatia idadi ya watu walioathiriwa na migogoro.

Bwana Ging ambaye amehitimisha ziara yake katika nchi hizo, ambayo pia ilimpeleka Kenya, amesema katika mahojiano na Redio ya Umoja wa Mataifa kuwa hali ya kibinadamu imeathiriwa na migogoro ya muda mrefu, huku hali ya hewa na mvua za El-Nino ikichangia kuongeza tishio la mzozo wa kibinadamu.

Nchini Sudan Kusini, amesema kuna ongezeko la asilimia 80 la idadi ya watu wasio na uhakika wa kuwa na chakula

“Kilichosababisha hiki ni kuchacha kwa mapigano na pia hali ya hewa- athari za El-Nino tayari zimeanza kuhisiwa. Kwa hiyo inatabirika, ina sura ya janga, na inaathiri vibaya sana watu”

Hata hivyo, amesema watu katika nchi hizo wanaonyesha ujasiri na uthabiti wa hali ya juu, akitolea mfano wa mji mmoja nchini Somalia

“Katika mji mmoja mdogo nchini Somalia uliokombolewa juzi kutoka kwa Al Shabaab baada ya miaka saba chini ya Al Shabaab, mahali paitwapo Hudua, kama mwendo wa saa moja kwa ndege kutoka Baidoa, ilihamasiaha kuona miradi ya wenyeji inayoendelezwa katika mji huo, kwa rasilmali ndogo sana. Ujumbe wao kwetu ulikuwa: tunasonga mbele na kazi yetu, tafadhali tusaidie. Msaada wenu utaleta tofauti kubwa.”

Kuhusu mahitaji ya kibinadamu kwa ujumla, Bwana Ging amesema

“Mahitaji yanafanana katika nchi zote ukizingatia mahitaji ya kibinadamu. Kwa waliolazimika kuhama- ambao ni mamilioni katika eneo zima – ni msaada wa chakula, huduma za afya, makazi, na pia panapowezekana, usaidizi wa kujikimu tena katika maisha yao. Tunachofanya katika huduma za kibinadamu ni kidogo sana, lakini ni sawa na tofauti kati ya uhai na kifo.”