Walinda amani 20 waachiliwa huru Sudan Kusini

Walinda amani 20 waachiliwa huru Sudan Kusini

Nchini Sudan Kusini, walinda amani 20 wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS wameachiliwa huru leo na waasi wa SPLM – upinzani.

Walinda amani hao walikuwa wametekwa nyara tangu jumatatu tarehe 26 mwezi huu, wakati moja ya boti za UNMISS zinazosafirisha mafuta kwenye mto wa Nile ilivamiwa na waasi wapatao 100.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari akielezea wasiwasi wa UNMISS kuhusu wafanyakazi wa kitaifa waliokuwa wakiendesha boti hiyo na ambao bado hawajaachiliwa huru.

Aidha waasi hao bado wamebaki na boti husika pamoja na vifaa na silaha za walinda amani.

Bwana Dujarric amesihi waliotekwa nyara waachiliwe huru bila kuteswa, akisema

(Sauti ya bwana Dujarric)

“Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unamwomba Riek Machar awajibike kama kiongozi wa SPLM – upinzani na atimize ahadi yake ya kuwarudisha wote kwa Umoja wa Mataifa kwa usalama”

Aidha amesema mashambulizi dhidi ya walinda amani na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa yanaweza kubainiwa kama uhalifu wa kivita.