Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na WFP zazindua upimaji wa viwango vya lishe kwa watoto Sudan Kusini

UNICEF na WFP zazindua upimaji wa viwango vya lishe kwa watoto Sudan Kusini

Wakati Sudan Kusini ikikabiliwa na tishio la njaa, Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF na lile la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, yamezindua kampeni ya kuchagiza umma kwa ajili ya kuwapima watoto zaidi ya robo milioni katika jimbo la Warrap, ili kutambua viwango vya utapiamlo.

Zaidi ya watu milioni 3.9 wanakabiliana na njaa kubwa nchini Sudan Kusini, huku tathmini mpya ikionya kuwa angalau watu wapatao 30,000 wanaishi katika hali mbaya sana, wakitishiwa na njaa na vifo.

Watoto wapatao 237,000 nchini Sudan Kusini wanakadiriwa kuwa na utapiamlo uliokithiri.

Kuanzia sasa hadi mwishoni mwa mwaka, wahudumu wa kujitolea wapatao 240 ambao wamepewa mafunzo na Wizara ya Afya ya jimbo kwa usaidizi wa UNICEF na WFP, wataenda nyumba hadi nyumba kupima zaidi ya watoto robo milioni, na kuwatuma wenye utapiamlo kwa vituo vya afya.