Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suala la kupunguza nyama zilizosindikwa laibua hoja:WHO

Suala la kupunguza nyama zilizosindikwa laibua hoja:WHO

Siku mbili baada ya shirika la kimataifa la utafiti kuhusu saratani, IARC kutoa ripoti yake ya uhusiano kati ya nyama zilizosindikwa na saratani ya utumbo mkubwa, shirika la afya duniani, WHO limesema limepokea idadi kubwa ya maswali na hoja zenye wasiwasi zinazotaka maelezo zaidi ya kina kuhusu chapisho hilo.

Taarifa ya WHO imesema kile ambacho utafiti huo umetoa, kimethibitisha mapendekezo yake ya mwaka 2002 kuhusu lishe na kinga dhidi ya magonjwa sugu iliyoshauri watu kupunguza matumizi ya nyama iliyosindikwa ili kupunguza hatari ya kupata saratani.

Hata hivyo WHO imesema chapisho hilo la IARC halilengi kuzuia watu kuacha kula nyama zilizosindikwa bali linadokeza umuhimu wa kupunguza bidhaa hizo ili kupunguza hatari ya kupata saratani ya utumbo mpana.

IARC ilianzishwa miaka 50 iliyopita kupitia azimio la WHO ikiwa ni mamlaka huru ya utafiti na kazi zake zinafadhiliwa na kuidhinishwa na nchi zinazoshiriki.