Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya raia 330 wakombolewa kutoka Boko Haram, UNICEF yazungumza

Zaidi ya raia 330 wakombolewa kutoka Boko Haram, UNICEF yazungumza

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limekaribisha hatua ya kukombolewa kwa raia zaidi ya 330 kutoka mikononi mwa kikundi cha kigaidi cha Boko Haram nchini Nigeria.

Mkuu wa masuala ya mawasiliano wa UNICEF nhini Nigeria Doune Peter ameiambia Radio ya Umoja wa Mataifa kuwa raia hao wengi wao wakiwa wanawake na watoto wamekombolewa kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la Nigeria dhidi ya ngome za Boko Haram nchini humo.

Amesema baada ya kuwa huru, raia hao wamepelekwa kwenye kambi ambako serikali inafanya ukaguzi kuhakikisha hakuna masalia ya Boko Haram na ndipo wanapelekwa kwenye maeneo ya kupatiwa misaada muhimu ikiwemo chakula, malazi na vifaa.

Douane amesema wengi wanawasili wakiwa na hali mbaya, mathalani watoto wanakuwa na utapiamlo, wanawake na watoto wa kike wamebakwa huku wengine wakiwa wajawazito an wengine wameambukizwa magonjwa ikiwemo virusi vya Ukimwi.

Kwa mantiki hiyo…

(Sauti ya Douane)

“Unicef na wadau wetu tumeweza kuwapatia haraka huduma za msingi za afya, baadhi yao pia wamejeruhiwa wakati wa mapigano ya kukombolewa kutoka Boko Haram. Pia tunawapatia huduma ya lishe kwa watoto ambao wana utapiamlo. Pia tunawapatia ushauri nasaha na hii ni muhimu sana kwani wameshuhudia mambo mabaya sana.”