Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO na FARDC kuanzisha operesheni kubwa dhidi ya ADF

MONUSCO na FARDC kuanzisha operesheni kubwa dhidi ya ADF

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, jeshi la taifa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO wameanzisha leo operesheni kubwa ya pamoja dhidi ya waasi wa ADF waliopo kwenye eneo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Radio Okapi, lengo la operesheni hiyo ni kuteketeza makazi ya waasi wasianzishe mashambulizi dhidi ya raia.

Tangu leo asubuhi wanajeshi wa serikali na MONUSCO wanarusha mabomu kwenye makazi ya ADF yaliyo karibu ya Beni, huku wananchi wakiripotiwa kuingiliwa na hofu kubwa.

Operesheni hiyo imezinduliwa wakati ambapo ripoti ya Umoja wa Mataifa imemulika kwamba ADF haijadhibitiwa, waasi wake wakiendelea kutesa raia kwenye eneo la Beni na Kivu Kaskazini ambapo watu wapatao 400 wameuawa kwa kipindi cha mwaka mmoja kutokana na mashambulizi yao.