Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa vipya vya Ebola vyaripotiwa Guinea

Visa vipya vya Ebola vyaripotiwa Guinea

Shirika la afya duniani, WHO limethibitisha visa vipya vitatu vya Ebola kwenye mkoa wa Forecariah, nchini Guinea. Taarifa kamili na Grace Kaneiya.

(Taarifa ya Grace)

Wagonjwa hao kutoka katika kaya moja wameripotiwa wiki iliyopita wakati ambapo nchi hiyo ilikuwa haina kisa chochote kipya kwa wiki tano mfululizo na imeelezwa kuwa wagonjwa hao kutoka familia moja walikuwa na magusano na mgonjwa wa Ebola.

WHO inasema wagonjwa hao ambao ni mwanamke mjamzito mwenye umri wa miaka 25, kwa sasa wanapatiwa matibabu pamoja na watoto wake wawili.

Kwa sasa shirika hilo linafuatilia watu 364 wanaoaminika kuambukizwa kirusi hicho, idadi ikiwa ni kubwa kuliko wiki iliyotangulia.

Kwa wiki 13 zilizopita, kiwango cha maambukizi ya Ebola kimekuwa si zaidi ya watu Watano nchini Guinea huku Sierra Leone ikiwa haina kisa chochote kipya kwa wiki sita mfululizo.

Iwapo Sierra Leona haitakuwa na kisa chochote kipya cha maambukizi hadi tarehe Saba mwezi ujao, itatangazwa kuwa imetokomeza Ebola.

Tangu Ebola iibuke mwezi Machi mwaka jana, imeua watu zaidi ya Elfu 11 wengi wao wakiwa ni kutoka Liberia, Sierra Leone na Guinea.