Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuonyeshe mbadala bora wa misimamo mikali kwa raia: Ban

Tuonyeshe mbadala bora wa misimamo mikali kwa raia: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyeko ziarani huko Hispania amehutubia mjadala wa kimataifa kuhusu kuzuia na kukabili misimamo mikali na kusema misimamo hiyo inazidi kuchochea ugaidi kote ulimwenguni.

Amesema vitendo hivyo vinazidi licha ya mikakati kadhaa iliyochukuliwa akitolea mfano ule wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wa mwaka 2006 uliolenga kudhibiti ugaidi kwa kuimarisha mfumo wa demokrasia duniani.

Ban amewaeleza washiriki kwenye kusanyiko hilo la Club de Madrid kuwa kama hiyo haitisho, misimamo hiyo mikali ni shambulizi la moja kwa moja kwa katiba ya Umoja wa Mataifa kwa kuwa inazorotesha amani kwa kuua raia, kubaka, kuuza wanawake kwenye utumwa wa kingono na hata kutesa raia.

Katibu Mkuu amesema harakati za kudhibiti misimamo mikali inasalia kuwa kipaumbele lakini kinga ni bora zaidi na haki za binadamu kwenye udhibiti zizingatiwe, na kubwa zaidi kwa wale wanaorubuniwa na kujiunga na vikundi hivyo..

(Sauti ya Ban)

“Lazima tuwaonyeshe mbadala bora zaidi. Hii inajumuisha kufanya kazi kutokomeza umaskini, ukosefu wa usawa na kuwapatia fursa. Na ina maana kuzingatia haki za binadamu na kuwapatia fursa za amani zaidi za kutatua machungu yao..”

Ban amesema hiyo ni muhimu kwa kuwa mara nyingi vikundi vyenye misimamo mikali hujinasibu kuwa suluhu la utawala usio bora na rushwa vinavyokuwa vinatekelezwa na serikali.