Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa OCHA aomba misafara ya usaidizi wa kibinadamu iruhusiwe kufikia wasyria

Mkuu wa OCHA aomba misafara ya usaidizi wa kibinadamu iruhusiwe kufikia wasyria

Baraza la Usalama leo limekuwa na mjadala maalum kuhusu hali ya kibinadamu mashariki ya kati na hasa Syria, huku mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA Stephen O’Brien akieleza kwamba sasa idadi ya watu wanaohitaji misaada ya kibinadamu nchini humo imefikia milioni 13.5.

Bwana O’Brien ameongeza kwamba vikwazo vinavyowekwa na serikali na vikosi vya upinzani dhidi ya misafara ya usaidizi wa kibinadamu huzuia mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake kufikia watu wanaohitaji msaada.

(Sauti ya Bwana O’Brien)

Tungeweza kuwafikia watu milioni 1.5 zaidi wanaohitaji msaada sana kwenye maeneo yasiyofikiwa kwa urahisi na maeneo yaliyozingirwa iwapo misafara ya pamoja ya mashirika ya kibinadamu ingekubaliwa na kuruhisiwa kupita kwa usalama.”

Aidha Bwana O’Brien amesema kwamba kuongezeka kwa mapigano na ghasia kwa kipindi cha wiki chache zilizopita kumesababisha idadi kubwa va  vifo, majeraha na kulazimisha watu wengi zaidi kukimbia makwao, huku akiongeza kwamba hali ya maisha imezidi kuwa mbaya kwa mamilioni ya wasyria wanaokosa huduma za msingi.

Akitoa wito kwa pande za mzozo na jamii ya kimataifa kufikia suluhu ya kisiasa kwa mzozo huo, amesema mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake wataendelea kujitahidi kutimiza mahitaji ya kibinadamu nchini humo, iwapo ufadhili utapatikana.