Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 45,000 wapata usaidizi kupitia ubia wa UNICEF na mfuko wa H&M

Watoto 45,000 wapata usaidizi kupitia ubia wa UNICEF na mfuko wa H&M

Zaidi ya watoto 45,000 wamenufaika kutokana na programu za maendeleo ya watoto wachanga, ECD na za elimu katika mwaka wa kwanza wa ubia kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF na mfuko wa H&M Conscious.

Ubia huo husaidia katika kutoa vifaa vya elimu, programu za lishe na fursa nyingine za kusoma katika jamii za mashinani ili kusaidia maendeleo ya watoto wenye umri chini ya miaka sita katika nchi za Benin, Jamhuri ya Lao, Mali, Nepal, Rwanda, na Timor Leste.

Kwa mujibu wa UNICEF, programu hizo pia zinatoa mafunzo kwa wazazi na walezi wapatao 600 nchini Mali kuhusu umuhimu wa kuhamasisha watoto kiakili na kijamii, na programu za mafunzo kupitia televisheni ya kitaifa inayowafikia makumi ya maelfu ya nyumba katika Jamhuri ya Lao.

UNICEF imesema ubia huo ni muhimu kwa sababu katika miaka sita ya kwanza, ubongo wa mtoto hukua haraka sana, na hivyo kuchangia jinsi atakavyokuwa kiakili, kihisia, kijamii na uwezo wa kusoma na kupata ufanisi katika maisha yao ya baadaye.