Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukuaji wa kiuchumi waporomoka Kusini mwa Jangwa la Sahara-IMF

Ukuaji wa kiuchumi waporomoka Kusini mwa Jangwa la Sahara-IMF

Ripoti mpya ya Shirika la Fedha Duniani, IMF, imesema kuwa shughuli za kiuchumi zimedhoofika kwa kiasi kikubwa barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, na kwamba nguvu ya kasi ya ukuaji wa miaka ya hivi karibuni imepungua katika nchi kadhaa. Taarifa kamili na Joshua Mmali..

(Taarifa ya Joshua)

Ripoti hiyo ya IMF inayomulika sura ya uchumi kanda ya kusini mwa jangwa la Sahara inakadiria ukuaji katika eneo hilo kuwa asilimia 3¾ mwaka huu, ikiwa ni chini ya ukuaji ulivyokuwa mwaka 2009 baada ya mdororo wa kifedha duniani.

Céline Allard, mkuu wa tafiti za kikanda katika IMF, na mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo ya IMF, na anasema baadhi ya sababu ya hali hii ni bei ndogo ya bidhaa na nchi nyingi kuwa na akiba ndogo ya fedha za kutumia kupiga jeki uchumi.

“Kwa hakika nchi nyingi zinaingia kipindi hiki zikiwa na upungufu mkubwa wa fedha kuliko zilivyokuwa wakati wa mdororo wa kifedha duniani”

Licha ya hali hiyo, kiwango cha ukuaji wa uchumi katika eneo hilo bado ni kikubwa zaidi kuliko maeneo mengine duniani. Bi Allard anaeleza ni kwa nini..

“Mosi, ni kuboreshwa kwa kiasi kikubwa kwa mazingira ya biashara. Sababu nyingine mbili ni bei ya juu ya bidhaa na hali iliyoimarika kifedha kimataifa hivi karibuni, ambayo imesaidia uwekezaji katika kanda hiyo. Sasa sababu hizo mbili zimefifia, na ndiyo maana tunaona kasi ikishuka.”