Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waunda ujumbe wa kuchunguza uvunjaji haki za binadamu Sudani Kusini

UM waunda ujumbe wa kuchunguza uvunjaji haki za binadamu Sudani Kusini

Kamishna  mkuu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein ameanza kuweka ujumbe nchini Sudan Kusini kwa ajili  ya kuendesha tathimini ya hali ya haki za binadamu nchini humo kufuatia ripoti za tuhuma za uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu unaodiwa kutekelezwa na pande kinzani nchini humo. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte.

(TAARIFA YA PRISCILLA)

Taarifa ya Kamishna Zeid inasema kuwa wajumbe watatu wa awali miongoni mwa kumi katika ujumbe wa tathimini wamewasili mjini Juba juma lililopita tayari kuanza kazi hiyo ambapo ujumbe huo utajikita zaidi katika uvunjifu wa haki za binadamu ambao umeathiri raia tangu kulipuka kwa machafuko nchini humo Disemba 2013.

Ripoti ya tathmini hiyo inatarajiwa kuwasilishwa katika baraza la haki za binadamu mwezi Machi mwaka 2016.

Zeid amesema timu ya uchunguzi itaangazia uvunjifu wa haki za binadamu za kimataifa na zile za kibinadamu  na kuongeza kuwa ripoti ya matokeo itajumuisha mapendekezo ya kuimarisha haki za binadamu nchini Sudan Kusini na kushauri baraza la haki za binadamu nini cha kufanya baadaye.

Amesema ripoti hiyo pia itabainisha umuhimu wa uwajibikaji panapotokea uvunjifu wa haki za binadamu.