Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaeleza wasiwasi wake kuhusu dhuluma ya kingono inayokumba wakimbizi na wahamiaji

UNHCR yaeleza wasiwasi wake kuhusu dhuluma ya kingono inayokumba wakimbizi na wahamiaji

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Wakimbizi, UNHCR,limeelezea wasiwasi wake kuhusu ushahidi wa kuaminika ambao imepokea juu ya vitendo vya wakimbizi na wahamiaji na watoto na wanawake kukumbwa na ukatili wa kingono wanapoelekea Ulaya.

Kwa mujibu wa UNHCR, hadi sasa, zaidi ya wakimbizi na wahamiaji 644,000 wamewasili Ulaya kwa njia ya bahari, na kati ya hao, asilimia 34 ni wanawake na watoto.

Hata hivyo yaelezwa kando mwa masaibu mengine yanayowakumba kabla ya kufika Ulaya, wanawake na watoto wanakabiliwa na hatari mbalimbali ikiwemo ukatili wa kingono.

Melissa Fleming ni msemaji wa UNHCR, Geneva.

(Sauti ya Melissa Fleming)

" Tumesikia ushuhuda wa kusikitisha sana unaoonyesha kwamba kuna matukio ya watoto kushiriki ngono ili kulipa wasafirishaji haramu waweze kuendelea na safari yao, au kwa sababu wameishiwa na fedha au kwa sababu wameibiwa"