Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majengo 300 yaangazia rangi ya buluu kwa miaka 70 ya UN

Majengo 300 yaangazia rangi ya buluu kwa miaka 70 ya UN

Zaidi ya majengo na minara 300 mashuhuri duniani kwenye nchi 75 yameangaza rangi ya buluu wakati ambapo Umoja wa Mataifa unaadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, tarehe 24 Oktoba.

Miongoni mwa majengo hayo maarufu yanayoangazia rangi ya buluu ambayo ni rangi rasmi ya Umoja wa Mataifa ni piramidi za Giza nchini Misri, Empire State jijini New York, Marekani, Yesu Mwokozi huko Rio je Janeiro nchini Brazil, na Ukuta mkubwa wa China na Ukumbi wa Kongamano wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC) mjini Nairobi, Kenya.

Akizungumza wakati wa kuwasha rangi ya buluu kwenye jengo la Empire state jijini New York Marekani, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema kawaida jengo hilo linamulika rangi za timu za michezo, lakini hivi Umoja wa Mataifa umekuwa kama timu ya kimataifa, ambayo inapenda kushinda katika kukuza amani, haki za binadamu na haki za binadamu.

Amesema Umoja wa Mataifa unapenda kushinda kwa ajili ya watu, na kwamba mwanga wa jiji la New York unashawishi kuadhimisha Umoja huo ambao ni mnara wa matumaini unaosaka kujenga mustakabali bora kwa wote.

Makao makuu ya Umoja wa Mataifa pia yataangazia rangi ya buluu leo na jumamosi tarehe 24 huku tumbuizo maalum la muziki likifanyika Ijumaa jioni.

Picha za tukio hilo zinapatikana kwenye mitandao ya kijamii kupitia akaunti ya Flickr (link), Twitter kupitia alama ya reli #UNblue na #UN70 na unifeed.