Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya haki za binadamu yashtushwa na mauaji ya raia Burundi

Ofisi ya haki za binadamu yashtushwa na mauaji ya raia Burundi

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imeelezea wasiwasi mkubwa kuhusu vurugu inayozidi kuongezeka nchini Burundi, ikisema watu wapatao 198 wameuawa tangu tarehe 26 April mwaka huu, theluthi moja kati yao wakiwa wameuawa katika kipindi cha wiki tatu zilizopita.

Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Rupert Colville amesema wametiwa wasiwasi zaidi na tukio la tarehe 13 mwezi huu kwenye eneo la Ngagara mjini Bujumbura, ambapo raia tisa waliuawa na polisi wakiwemo mwandishi wa habari na familia yake na mfanyakazi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM.

(Sauti ya bwana Colville)

“ Licha ya ripoti zingine za mashambulizi dhidi ya wahudumu wa kibindamu, ni mara ya kwanza mhudumu wa kibinadamu anauawa na polisi tangu mwanzo wa mzozo. Tunasihi mamlaka zipatie miongozo vikosi vyote vya usalama kuwa vitendo kama hivyo vitaadhibiwa kisheria.”

Kadhalika Bwana Colville amesema ofisi yake inakaribisha hatua ya ofisi ya mwanasheria wa serikali ya kuunda tume ya uchunguzi kuhusu tukio hilo, akiomba uchunguzi huo uwe wa uwazi na haki..