Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtalaam huru kuhusu ualbino atoa mapendekezo

Mtalaam huru kuhusu ualbino atoa mapendekezo

Mtalaam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu walemavu wa ngozi, Albino, Bi. Ero Ikponwosa,amesema changamoto zinazokumba watu hao si tu mashambulizi bali pia unyanyasaji na ubaguzi ambao pia huhatarisha maisha yao. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Akihutubia mkutano wa kamati ya tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Bi Ero amesema ubaguzi dhidi ya watu wenye ualbino hukumba zaidi watu barani Afrika kwa sababu ya tofauti kubwa ya rangi na makali ya jua yanayoathiri ngozi zao na hivyo kuwafanya kuonekana zaidi kwenye jamii.

Amesema mashambulizi na biashara ya viungo vya mwili vya albino hutokea katika nchi takriban 25 na kuhusishwa na imani za kishirikina.

Kwenye mahojiano na idhaa hii, bi Ero ameelezea mapendekezo anayotarajia kupeleka mbele ya ofisi ya haki za binadamu.

(Sauti ya Bi Ero)

“ Lazima kuelimisha jamii, hasa vijijini, kupitia viongozi wa jamii, hasa waganga wa kyenyeji. Kwa sababu iwapo waganga hawa wanaotumia uchawi wapo, shida ipo. Pia kuwahudumia watoto wenye ualbino shuleni ili waweze kuona na kusoma. Hatimaye kushughulikia swala la afya, ili kutokomeza mlipuko wa saratani ya ngozi, kwani wengi wanakufa kati ya umri wa miaka 30 na 40, na mlipuko huo unaweza kusitishwa.”