Dola Milioni 12 kusaidia CAR: OCHA

Dola Milioni 12 kusaidia CAR: OCHA

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya usaidizi wa kibinadamu, Stephen O’Brien ambaye anahitimisha ziara yake huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR ametangaza kutoa dola Milioni 12 kwa ajili ya kuokoa maisha ya raia wa nchi hiyo.

Taarifa ya ofisi anayoongoza ya usaidizi wa binadamu, OCHA imesema fedha hizo kutoka mfuko wa dharura, CERF ni kwa ajili ya operesheni za kibinadamu lakini fedha zaidi zinahitajika.

Pamoja na kutangaza fedha hizo, Bwana O’Brien ametoa wito kwa raia kulindwa zaidi nchini humo wakati huu ambapo janga la kibinadamu linazidi kushika kasi nchini humo.

Amesema hatua zahitajika kuiokoa CAR kwa kuwa siyo tu wananchi wanataabika bali pia ghasia zinaongezeka na kuzuia utawala bora huku  uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu ukikumbwa na vikwazo.

Ziara hiyo ya tangu tarehe 20 mwezi huu imemkutanisha na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali, mashirika ya kimataifa na wananchi,ambapo Bwana O’Brien ameweza kuzungumza na wakimbizi wa ndani huko Dekoa waliomweleza jinsi walikimbia ghasia na wanachotaka sasa ni usalama warejee makwao.

O’Brien amekuwa afisa wa kwanza wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa kutembelea CAR tangu ghasia zizuke tena mwezi Septemba mwaka huu na kusababisha zaidi ya watu Elfu 62 wakimbie makazi yao.