Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

El Nino yaweza kufanya hali ya kipindupindu Tanzania kuwa mbaya zaidi:WHO

El Nino yaweza kufanya hali ya kipindupindu Tanzania kuwa mbaya zaidi:WHO

Shirika la afya duniani, WHO limesema lina wasiwasi mkubwa juu ya mlipuko wa Kipindupindu nchini Tanzania wakati huu ambapo utabiri wa hali ya hewa unaashiria mvua kubwa za El Nino.

Mfuatiliaji mkuu wa masuala ya kipindupindu ndani ya WHO Dkt. Dominique Legros amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuwa ugonjwa huo sasa umeenea katika mikoa 14 pamoja na kisiwa cha Unguja huko Zanzibar.

Amesema mji wa Dar es salaam unaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa ambao ni 3,500 tangu mwezi Agosti na kati yao 74 wamefariki dunia na chanzo ni..

(Sauti ya Dkt. Legros)

“Changamoto ya kupata maji safi na salama, ni mji mkubwa wenye makazi duni mengi. Kimo cha maji ardhini kiko juu na hivyo inakuwa vigumu kupata maji na kujenga vyoo. Hofu yetu kwenye eneo hilo ni utabiri wa hali ya hewa unaoonyesha msimu wa mvua nyingi sana za El Nino mapema mwakani.”

Mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Alvaro Rodriguez amesema wanasaidia serikali akigusia suala la wauza vyakula na maji.

(Sauti ya Alvaro)

“Ambako tunaamini ndiko mlipuko ulianzia na biashara hiyo inachangia kuzidi kuenea. Sasa hivi tunashirikiana na OCHA kupata fedha na tunajua tunaweza kudhibiti mlipuko.”

Nchi zingine ambazo mlipuko wa Kipindupindu umeriporitwa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Iraq, Bahrain na Kuwait.