Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwakilishi wa UN Libya asisitiza utaratibu wa amani unaendelea licha ya sintofahamu

Mwakilishi wa UN Libya asisitiza utaratibu wa amani unaendelea licha ya sintofahamu

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Bernadino Leon amesema utaratibu wa amani unaendelea licha ya tangazo kutoka kwa baadhi ya wabunge lililopinga makubaliano ya amani yaliyoafikiwa wiki mbili zilizopita kuhusu uundaji wa serikali jumuishi.

Akiongea leo na waandishi wa habari mjini Tunis, nchini Tunisia, bwana Leon amesema tangazo hilo limesababisha mashaka na amesisitiza kuwa hatakubali vikundi vya viongozi wachache kuharibu utaratibu huo wa amani ambao unategemewa na wengi wa walibya.

Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa amesema raia wa Libya ndio wanaoteseka zaidi na sintofahamu hizo na kwamba ni wajibu wa jamii ya kimataifa na wadau wa kisiasa kusitisha mateso yao.

Aidha amesisitiza kuwa utaratibu huo umekuwa jumuishi, ukishirikisha wadau wote wa Libya pamoja na wawakilishi wa jamii, na kuwa si chaguo la Umoja wa Mataifa.

Hatimaye ameelezea mwelekeo:

(Sauti ya Bwana Leon)

“ Tutaitisha mikutano mipya siku zijazo ili kusikiliza mapendekezo na maoni ya walibya walioshiriki kwenye utaratibu huo na wale ambao hawakushiriki, ili tuendelee, kwa sababu ni lazima tuwe na serikali ya umoja mjini Tripoli, ambayo inatuma ujumbe za faraja kutoka Tripoli. Ni muhimu walibya waone kwamba tunaendelea na kwamba mapendekezo kutoka utaratibu huo yatashinda.”