Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na ujumbe wa utetezi wa watoto kupitia kriketi

UNICEF na ujumbe wa utetezi wa watoto kupitia kriketi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwa kushirikiana na baraza la kimataifa la kriketi ICC wametangaza leo ubia katika utetezi kwa watoto wanaokosa fursa kote duniani.

Kila mwaka zaidi ya watoto milioni tano hufa kabla ya kuadhimisha miaka mitano ya kuzaliwa kutokana na sababau ambazo zaweza kuzuilika, nusu bilioni wakiishi katika umasikini uliokithiri na wengine zaidi ya milioni 50 waliofikisha umri wa kwenda shule hawajajiunga.

Ubia huo uliopewa jina Kriketi kwa mema unalenga kutoa elimu kwa uma kuhusu changamoto zinazowakabili watoto na kuhamasisha mashabiki wa mchezo huo kuzungumza kwa niaba ya watoto ambao maisha yao ni sehemu ya takwimu tajwa.

Ubia wa UNICEF na ICC unatarajiwa kutumia jukwaa la mchezo wa kriketi ambao ndiyo unaotizamwa zaidi nchini India, kuwafikia watu na ujumbe wa utetezi kwa watoto. Nchi zinazopenda mchezo huo pia zitafikiwa.  Mashindano  ya kriketi ya dunia mwaka 2015 ndiyo yameshika rekodi ya kutazamwa zaidi nchini India kupitia runinga ambapo zaidi ya watu milioni 600 walitazama.