Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mzozo Mashariki ya kati, suluhu mikononi mwa Israeli na Palestina: Ban

Mzozo Mashariki ya kati, suluhu mikononi mwa Israeli na Palestina: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon bado yuko Mashariki ya Kati akisaka suluhu ya mzozo kati ya Israeli na Palestina ambapo leo amekuwa na mazungumzo na Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas. Assumpta Massoi na taarifa zaidi.

(Taarifa ya Assumpta)

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Ramallah, mkutano uliohudhuriwa pia na Bwana Abbas, Katibu Mkuu ameeleza wasiwasi wake juu ya kuendelea kwa mvutano kati ya pande mbili hizo kwenye maeneo ya Palestina yanayokaliwa na Israel.

Amerejelea tena kuwa ghasia siyo suluhu na kwamba uamuzi wa upande mmoja kujichukulia hatua, ni kukwamisha mafanikio yote yaliyopatikana katika kujenga msingi wa kuwa na mataifa mawili pamoja ambayo ni Israeli na Palestina.

Amesema hata kama jamii ya kimataifa inasaka kusaidia lakini hatma ya amani ya kudumu ni uamuzi wa wapalestina na waisraeli wenyewe.

“Changamoto ya dharura ni kusitisha wimbi la sasa la ghasia na kuepusha vifo zaidi vya watu. Ninasikitishwa sana na uchochezi kwenye maeneo matakatifu Yerusalem, uchochezi ambao umesababisha mlipuko wa ghasia za sasa. Kushughulikia mvutano wa sasa ni muhimu ili kubadili mwelekeo na hivyo zisiendelee. Nakaribisha hakikisho la mara kwa mara la Israel kuwa haina nia ya kubadili umiliki wa maeneo ya kihistoria na matakatifu. Katika mazungumzo yangu jana na maafisa wa Israel nimesisitiza kuwa ni kupitia vitendo thabiti kwenye eneo husika ndio mtazamo utabadilika.”

Ban amesema matumaini yake ni kwa uongozi na azma yao ya kuleta amani na utulivu kwenye eneo hilo ambako hatma ya uwepo wa mataifa mawili inaweza kufikiwa muda si mrefu.