Dola Milioni 60 zahitajika kunusuru afya Yemen:WHO
Shirika la afya duniani, WHO limesema kuendelea kudorora kwa hali ya usalama nchini Yemen,hususan katika jimbo la Taiz kumezidi kukwamisha operesheni zake za kutoa huduma za msingi za afya.Taarifa zaidi na Grace Kaneiya.
(Taarifa ya Grace)
Taarifa ya WHO imesema huko Taiz, watu zaidi ya Milioni Tatu wakiwemo wakimbizi Laki Tatu wanahitaja huduma za dharura za kiafya lakini ukosefu wa usalama ni kikwazo cha kuwafikia.
Mwakilishi wa WHO nchini Yemen Dkt. Ahmed Shadoul amesema mahitaji kama vile maji safi na salama na dawa kwa matibabu ya kipindupindu ni muhimu na kwamba kila uchao mahitaji yanaongezeka.
Kwa mantiki hiyo amesema ili kuendelea na operesheni zao nchini Yemen hadi mwishoni mwa mwaka huu, watahitaji dola Milioni 60 na tayari wameshatoa tani 30 za dawa na vifaa tiba kwa jimbo la Taiz.