Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lafanya mjadala wa wazi kuhusu utendaji kazi wake

Baraza la Usalama lafanya mjadala wa wazi kuhusu utendaji kazi wake

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, leo limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu mbinu zake za utendaji kazi.

Katika mkutano huo, wajumbe wa Baraza la Usalama wamepata fursa ya kuzungumzia masuala yanayohusu utendaji kazi bora, na pia kukosoana kuhusu mbinu zisizofaa.

Akihutubia Baraza hilo, Naibu Katibu Mkuu, Jan Eliasson, amesema watu duniani wanapofikiria kuhusu Umoja wa Mataifa, mara nyingi wanafikiria kuhusu Baraza la Usalama..

“Mna wajibu mzito wa kudumisha amani na usalama wa kimataifa katika dunia yenye matatizo, tata na inayohusiana. Matarajio ya watu kwenu ni makubwa kote duniani. Ndiyo maana mjadala kuhusu utendaji kazi wenu unawavutia wengi.”

Akizungumza kuhusu uhusiano wa sekritariati ya Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama, Bwana Eliasson amesema Idara ya Masuala ya Kisiasa katika Umoja wa Mataifa imeanzisha desturi ya kulihutubia Baraza la Usalama kila mwezi kuhusu hali ambazo zinaweza kugeuka kuwa matishio kwa amani na usalama wa kimataifa.

Kwa mantiki hiyo, amesema ishara za mapema za onyo zinaweza na zinapaswa kuchangia hata zaidi katika kuzuia hali kuzorota au kuwa isiyoweza kudhibitika.

Akihitimisha, Bwana Eliason amewashukuru wajumbe wa Baraza la Usalama, akisema:

“Tumefurahishwa na uwazi ulioonyeshwa katika mchakato wa leo. Kazi ya Baraza la Usalama inaathiri nchi zote wanachama na watu duniani, ambako amani, maendeleo na haki za binadamu vinazidi kuwa na uhusiano.”