Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwekaji bora wa takwimu ni muhimu katika kutimiza SDGs- Ban

Uwekaji bora wa takwimu ni muhimu katika kutimiza SDGs- Ban

Ikiwa leo ni siku ya takwimu duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana ili kuhakikisha kuwa uwekezaji unaofaa unafanywa, uwezo stahiki wa kitaaluma unaimarishwa na mbinu bunifu zinatumiwa, ili kuzipatia nchi zote mifumo ya kina ya habari zinazohitajika ili kutimiza maendeleo endelevu.

Katika ujumbe wake kwa siku hii, Ban amesema takwimu bora ni sehemu isiyoweza kupuuzwa na wadau wote katika jamii, katika harakati za kufanya maamuzi yenye busara. Ameongeza kuwa ndiyo maana Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitambua umuhimu wa takwimu, na hivyo kupitisha kanuni za msingi za takwimu rasmi, ili kuendeleza haki ya raia kupata habari za umma.

Katibu Mkuu amesema katika jitihada za kutimiza ajenda kabambe ya maendeleo endelevu, 2030, takwimu zinazoweza kutegemewa na kutolewa kwa haraka ni muhimu hata zaidi, na ndiyo maana kauli mbiu ya mwaka huu ni: “takwimu bora, maisha bora”