Palestina na Israel, ghasia hazitaleta suluhu:Ban

Palestina na Israel, ghasia hazitaleta suluhu:Ban

Salaam Aleykum, Shalom! Leo, ningependa kuzungumza moja kwa moja kwa moja na watu wa Israel na Palestina kuhusu kuongezeka kwa machafuko kote katika maeneo ya Wapalestina yaliyokaliwa na Israel.

Ndivyo alivyoanza ujumbe wake wa Video, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mtataifa Ban Ki-moon wakati huu ambapo ghasia zinaripotiwa kila uchao kwenye eneo hilo.

Amesema anashangazwa kama kila mtu anavyopaswa kushangazwa anaposhuhudia vijana na watoto wakitwaa silaha na kutaka kuua. Ban amesema bayana kuwa, machafuko yatadhoofisha tu matakwa halali ya Wapalestina ya utaifa, na tamaa ya Waisraeli kuwa na usalama. Hivyo akatoa ujumbe kwa vijana wa Palestina.

(Sauti ya Ban)

“Naelewa kukata tamaa kwenu. Najua matumaini yenu ya amani yamevunjwa mara nyingi. Mna hasira kwa kukaliwa na kupanuliwa kwa maeneo ya kukaliwa. Wengi wenu hamjafurahishwa na viongozi wenu, pamoja nasi, jamii ya kimataifa kwa sababu hatujaweza kuumaliza mzozo huu.Na kwa viongozi wa Palestina, nasema hivi:Unganisheni nguvu za watu wenu kwa njia ya amani ili kuwawezesha kufikia ndoto matamanio yao. Mna haki ya kuishi maisha mema na kwa utu, heshima na uhuru.”

Ban akawa pia na ujumbe kwa watu na viongozi wa Israel…..

“Ningependa kusema kuwa natambua hofu yenu kuhusu amani na usalama. Naelewa pia hasira wanayohisi Waisraeli wengi. Watoto wanapoogopa kwenda shule, wakati mtu yeyote mtaani aweza kuwa mhanga, usalama ni jambo halali la kipaumbele.Lakini kuta, vituo vya upekuzi, hatua kali za vikosi vya usalama na uharibifu wa nyumba, haviwezi kuendeleza amani na usalama mnaohitaji na mnaostahili kupata.”

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa hakuna chochote kiitwacho suluhu la kiusalama na hivyo amesihi waisrael kama alivyofanya kwa wapalestina kuona nuru ya kisiasa na kuvunja mzunguko wa machafuko na uoga. Ban amesema Umoja wa Mataifa upo pamoja na pande hizo na utaendelea kuunga mkono juhudi za kuweka mazingira ya kurejelea mashauriano yenye maana na kwamba hakuna kukata tamaa.