Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN@70, Kenya miongoni mwa nchi zitakazoangaza buluu

UN@70, Kenya miongoni mwa nchi zitakazoangaza buluu

Jumla ya majengo na minara mashuhuri kutoka nchi 60 duniani itaangaza rangi ya buluu siku ya tarehe 24 Oktoba usiku ikiwa ni kilele cha miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa mawasiliano kwenye umoja huo Cristina Gallach amesema majengo na minara hiyo iko Australia, Asia, Afrika, Ulaya na Amerika.

Barani Afrika nchi Tisa zinashiriki zikiwemo Kenya kupitia kituo chake cha kimataifa cha mikutano cha Kenyatta, KICC, Piramidi za Giza huko Misri na Milima Meza ya huko Cape Town Afrika Kusini.

Bi. Gallach amesema mpango huo uliobuniwa na idara yake umeungwa mkono na serikali kuu na serikali za mitaa wakiwemo mameya kwa lengo la kuelimisha kuhusu siku ya Umoja wa Mataifa na kwamba kuhusu matumizi ya nishati kwenye maeneo hayo...

(Sauti ya Gallach-1)

“Kwamba tulipozindua mradi huu tuliziomba mamlaka za nchi husika zihakikishe kuwa nishati itakayotumika kuangazia rangi ya buluu inakuwa ni kidogo na kwamba huo mwanga wa buluu utumie nishati kidogo, na ni matumaini yetu kuwa hilo litazingatiwa.”

Umoja wa Mataifa ulianzishwa tarehe 24 Oktoba mwaka 1945 huko San Fransisco, Marekani ukiwa na wanachama 51 na sasa idadi ya wanachama imeongezeka na kufikia 193.