Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM na usaidizi kwa nchi zilizo na uhaba wa chakula Afrika

UM na usaidizi kwa nchi zilizo na uhaba wa chakula Afrika

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamechukua hatua kukabiliana na ukosefu wa uhakika wa chakula katika nchi za Kusini mwa Afrika.

Miongoni mwao ni lile la mpango wa chakula duniani, WFP na lile la chakula na kilimo FAO ambapo yamesema katika miezi sita ijayo, watu wapatao Milioni 27 watakumbwa na ukosefu wa chakula, yakinukuu tathimini za jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika, SADC.

Tathmini hizo zimeonyesha kuwa athari za El nino zitashika kasi zaidi mwishoni mwa mwaka huu huku ukosefu wa mvua na mavuno haba navyo vikitajwa kuchochea lishe duni miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

Nchi zilizotajwa kuwa hatarini zaidi ni Malawi, Zimbabwe na Madagascar ambapo Lesotho na Msumbiji nazo zina dalili za uhaba wa chakula zinazotiwa wasiwasi.

Tayari WFP na FAO zimechukua hatua kukwamua Malawi ambayo watu wake Milioni Mbili nukta Nane hawana uhakika wa chakula.

Hatua hizo ni pamoja na kusambaza mgao wa chakula na kushirikiana na serikali ya Malawi kuandaa mpango wa kitaifa wa kuchukua hatua dhidi ya ukosefu wa chakula.

Nchini Zimbabwe nako FAP inashirikiana na serikali kusaidia kuweka sera za jamii kuweza kukabiliana na mazingira yanayosababisha ukosefu wa chakula.

Hatua hizo ni pamoja na kusaidia jamii za wafugaji kushiriki katika ufugaji wa kisasa wa biashara na wakulima kupatiwa teknolojia stahimilivu kwa mabadiliko ya tabianchi.