Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

APRM kichocheo cha utawala bora Afrika: Dkt. Mayaki

APRM kichocheo cha utawala bora Afrika: Dkt. Mayaki

Afisa Mtendaji Mkuu wa mpango mpya wa ushirikiano kwa maendeleo ya Afrika Nepad, Dkt. Ibrahim Mayaki, ametaja mambo ya kuzingatiwa ili kuweza kufanikisha ajenda ya maendeleo endelevu, SDG sambamba na ile ya Afrika ajenda 2063.

Akihutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa katika mjadala wa pamoja kuhusu NEPAD na harakati za kutokomeza Malaria barani Afrika ikiwa ni sehemu ya hitimisho la wiki ya Afrika ndani ya Umoja wa Mataifa, Dkt. Mayaki ametaja mambo hayo kuwa ni utawala bora, elimu bora kwa wote, uwezeshaji wanawake, matumizi ya sayansi na teknolojia, miundombinu imara miongoni mwa machache.

(Sauti ya Dkt. Mayaki)

“SDGs ni msingi mzuri kwa suluhu za muda mrefu na endelevu ambazo zitawezesha Afrika kufikia matamanio yake ya maendeleo yaliyoelezwabayana kupitia NEPAD. Hata hivyo ni muhimu kuendeleza uoanishi wa SDGs au ajenda 2030 na ajenda 2063 ya Afrika na mpango wake wa miaka 10 wa utekelezaji utakaosimamiwa na NEPAD.”

Katika kusisitiza utawala bora akagusia mpango wa nchi za Afrika kujitathmini, APRM ulioasisiwa miaka 12 iliyopita akisema ni msingi wa ustawi barani Afrika kwani unasaidia kuimarisha demokrasia na kuakisi azma ya nchi hizo kuimarisha utawala bora.

Hata hivyo amesema..

“Kuelekea mbele, jukumu la haraka la APRM ni kutekeleza kwa dhati mipango ya utekelezaji ya kitaifa inayoandaliwa baada ya nchi kufanyiwa tathmini.”

Hadi sasa nchi 35 kati ya 54 wanachama wa Muungano wa Afrika zilijiunga kwa hiari na zoezi la APRM na 17 kati yao zinaingia katika awamu ya pili.