Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa Geneva watoa mapendekezo ya kubadili ajenda ya Kibinadamu

Mkutano wa Geneva watoa mapendekezo ya kubadili ajenda ya Kibinadamu

Washiriki zaidi ya 1,000 kutoka kote duniani leo wamehitimsha siku tatu za majadiliano kuhusu hatma ya misaada ya kibinadamu, kuimarisha na kuboresha maudhui na vitendo kwa sababu ya mabadiliko makubwa ya ajenda ya kushughulikia mahitaji ya kibinadamu yanayozidi kuongezeka duniani.

Akizungumza baada ya mkutano huo uliofanyika mjini Geneva, nchini Uswisi, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Elliason amesema, mkutano huo umetunga wito mwafaka wa kuwaweka watu katika mstari wa mbele katika ajenda ya kimataifa, hatua chachu kabla ya Mkutano wa Dunia wa Kibinadamu utakaofanyika Uturuki  23-24 Mei, 2016.

Halikadhalika, Elliason amesema, mashauriano ya wakati mwafaka ya mkutano huo, yametoa wito wa uongozi wa kutekeleza mageuzi kuhusu jinsi ya kutoa misaada ya binadamu kwa watu wanaoihitaji.

Aidha, Naibu huyo wa Katibu Mkuu amesema, ni lazima kuzingatia mapendekezo mengi muhimu yaliyotolewa wakati wa mashauriano na hivyo kufikia mapendekezo ya msingi kwa ajili ya Mkutano wa Istanbul.