Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malaria yaangaziwa mwishoni mwa wiki ya Afrika

Malaria yaangaziwa mwishoni mwa wiki ya Afrika

Wiki ya Afrika ndani ya Umoja wa Mataifa imehitimishwa leo kwenye makao makuu ya umoja huo jijini New York, Marekani kwa kufanyika mjadala wa pamoja kuhusu ubia mpya wa maendeleo barani humo, NEPAD na harakati za kutokomeza malaria hususan Afrika. Taarifa zaidi na Joseph Msami.

(Taarifa ya Joseph)

Bara la Afrika limekuwa likionyesha matumaini ya ustawi kutokana na maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii lakini bado Malaria inaendelea kuwa mwiba kwa wakazi wengi wa eneo hilo, amesema Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Mogens Lykketoft wakati akifungua mjadala huo.

Amesema ugonjwa huo licha ya kwamba una kinga na tiba bado unakwamisha maendeleo ya baadhi ya nchi za bara hilo zilizo na kiu ya kusonga mbele hivyo amesema..

(Sauti ya Mogens)

Tunapoanza sura mpya ya ushirikiano wa kimataifa kuna umuhimu pia wa kufanya kazi pamoja kukabili malaria, kulinda haki za binadamu na kuweka msingi wa amani, ustawi na maendeleo endelevu katika bara zima la Afrika.”

Akizunguma kwa niaba ya kundi la nchi 77 na China, mjumbe kutoka Afrika Kusini kwenye Umoja wa Mataifa Thulani Nyembe amesisitiza usaidizi dhidi  ya Malaria

(Sauti ya Mwakilishi)

Kuna umuhimu wa dhati kwa Umoja wa Mataifa hususan shirika la afya duniani lisaidie kuboresha mifumo dhaifu ya afya na ukosefu wa huduma za kutosha za afya.”