Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mratibu wa masuala ya kibinadamu CAR alaani shambulizi dhidi ya timu ya MSF

Mratibu wa masuala ya kibinadamu CAR alaani shambulizi dhidi ya timu ya MSF

Mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Aurélien A. Agbénonci na wadau wote wa kibinadamu nchini humo, wamelaani vikali shambulizi dhidi ya timu ya madaktari wasio na mipaka, MSF usiku wa tarehe 14 na 15 Oktoba, kule Bangassou, mkoa wa Mbomou.

Taarifa ya Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu, OCHA imesema, watu wasiojulikana walivamia majengo ya MSF saa nne usiku, wakawashambulia wafanyakazi na kuwateka wanne kati yao, ambao waliachiliwa dakika 30 baadaye.

Mfanyakazi mmoja wa kimataifa alijeruhiwa vibaya katika shambulizi hilo, lakini hali yake imetengamaa kufuatia upasuaji wa dharura.

Akilaani shambulizi hilo, Bwana Agbénonci ametoa wito kwa vikundi vyote vyenye silaha kuheshimu uhai na uhuru wa kutembea wa wafanyakazi wa kibinadamu ambao wanatoa usaidizi kwa watu walioathiriwa na mzozo nchini CAR.

Jens Laerke ni msemaji wa OCHA, Geneva

"Kwa sasa hatuna taarifa kuhusu waliotekeleza uhalifu huo, tunachojua ni kwamba ni watu waliokuwa wamejihami kwa visu na mapanga wakati walipoingia katika majengo hayo na ni kana kwamba hawana uhusiano na kundi lolote lilojihami nchini CAR kwa hiyo tunawachukulia kama wahalifu."