Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa ni zaidi ya kutokuwa na chakula- Ban

Njaa ni zaidi ya kutokuwa na chakula- Ban

Ikiwa leo ni Siku ya Chakula Duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, amesema kuwa na njaa siyo kukosa chakula tu, bali pia ni kukosa haki. Taarifa kamili na Assumpta Massoi

(Taarifa ya Assumpta)

Ban amesema hayo mjini Milan, Italia, katika sherehe ya kuadhimisha siku hii, ikiwa sehemu ya maonyesho ya Milan kuhusu chakula. Katibu Mkuu amesema siku hii ni ya kutoa ahadi ya kufikia uhakika wa chakula kwa wote, na kujenga vuguvugu la kimataifa la kutokomeza njaa.

Aidha, mapema leo akiwa mjini Turin, Italia Katibu Mkuu amehutubia kongamano la kimataifa kuhusu maendeleo ya kiuchumi mashinani, akisema wakati dunia ikimulika mikataba ya kimataifa, inapaswa ieleweke kuwa mazingira ya kitaifa ni muhimu katika kufanikisha jitihada za maendeleo ya kimataifa.

Ban amesema kufanikisha malengo 17 ya maendeleo endelevu kutatimizwa tu iwapo serikali na jamii mashinani zitashirikiana.

“Ndiyo maana ni muhimu sana kwa malengo haya ya kimataifa kuendelezwa mijini, mikoani na kikanda. Maendeleo ya uchumi mashinani huinua viwango vya maisha. Huendeleza ujumuishaji wa kijamii, na hivyo kuchangia ustawi na amani.”

Aidha, Ban amesema ili kuhakikisha maisha yenye utu kwa wote, ni lazima kuhakikisha kuna huduma bora za afya, elimu bora zaidi, usawa wa jinsia na mambo mengine yanayohusu maisha ya uhuru na usalama.