Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tupandacho, tuvunacho na tulacho kubainisha mustakhbali wetu;Ban

Tupandacho, tuvunacho na tulacho kubainisha mustakhbali wetu;Ban

Ulinzi wa kijamii na kilimo, tokomeza umaskini vijijini, ndio maudhui ya siku ya chakula duniani inayoodhimishwa hii leo ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ni mujarabu katika kuhakikisha jamii za vijijini zinakuwa endelevu na kuimarisha vipato vyao.

Katika ujumbe wake Ban Ki-moon amesema licha ya mafanikio katika kutokomeza njaa baadhi ya maeneo duniani, bado watu Milioni 800 wengi wao wakiwa vijijini wanakabiliwa na njaa.

Amesema hiyo inatokea wakati kuna watu ambao wana chakula cha kutosha na hata kutupa mabaki na hivyo kudhihirisha kuwa kasi ya kuondokana na njaa na umaskni bado ni ya kusuasua kwa wakazi wengi duniani.

Kwa mantiki hiyo Ban amesema ni lazima kufahamu kuwa uamuzi aina ya mazao ya kupanda, usindikaji, usambazaji na ulaji una athari katika ustawi wa watu, sayari, na amani.

Amesema njaa ni zaidi ya ukosefu wa chakula hivyo katika siku ya chakula duniani kila mmoja asisitize azma ya kushirikiana kutokomeza njaa duniani kwa mujibu wa lengo namba mbili la malengo ya maendeleo endelevu.