Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uruguay, Senegal, Japan, Ukraine na Misri zaingia Baraza la Usalama

Uruguay, Senegal, Japan, Ukraine na Misri zaingia Baraza la Usalama

Upigaji kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kuchagua wanachama watano wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la umoja huo umekamilika ambapo nchi zote nne ambazo ni Uruguay, Senegal, Misri, Ukraine na Japan zimepata kura za kutosha kuweza kujumuika kwenye chombo hicho kwa kipindi cha miaka miwili.

Wagombea hao hawakuwa na wapinzani katika ukanda wanaowakilisha na hivyo baada ya upigaji kura kukamilika matokeo ni kwamba Senegal imepata kura 187, Uruguay 185, Japan 184, Misri 179 na Ukraine 177.

Rais wa Baraza Kuu Mogens Lykketoft ambaye alikuwa ndiye mwenyekiti wa uchaguzi akasema…

(Sauti ya Lykketoft)

Baraza tayari limeidhinisha matokeo. Baada ya kupata idadi ya kura zinazotakiwa ambazo ni theluthi mbili na idadi kubwa ya kura, Misri, Japan, Senegal, Ukraine na Uruguay zimechaguliwa kuwa wanachama wa Baraza la Usalama kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Januari Mosi mwaka 2016.”

Misri na Senegal zinawakilisha kanda ya Afrika, huku Japan ikiwakilisha Asia, Ukraine kanda ya Ulaya Mashariki, na Uruguay kanda ya Amerika Kusini na Karibia.

Baraza lau usalama linaundwa na wajumbe 15 ambapo watano ni wa kudumu na 10 hawana ujumbe wa kudumu na uhudumu kwa kipindi cha miaka miwili miwili.