Skip to main content

Mshikamano na uongozi wenye kujali ndio siri ya kukabili changamoto:Ban

Mshikamano na uongozi wenye kujali ndio siri ya kukabili changamoto:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyeko ziarani nchini Italia amehutubia bunge la nchi hiyo na kusema kuwa chombo hicho kama vile wanachama wake kinakabiiliwa na changamoto ambazo kama ilivyo kwa wanachama wake hakiweza kuzikabili peke yake.

Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na zile za amani na usalama, majanga ya kibinadamu na hata ukiukwaji wa haki za binadamu akisema mshikamano baina ya taasisi hiyo na uongozi wenye kujali ndiyo siri pekee ya kuweza kuzikabili.

Kwa mantiki hiyo amekaribisha uhusiano wa miaka 60 kati ya Umoja wa Mataifa na Italia akisema umesaidia kusongesha malengo ya Umoja huo ikiwemo ulinzi na amani akitaja kuwa Italia ndiyo nchi ya magharibi inayoongoza kwa kuchangia walinda amani.

Ban pia ametumia hotuba yake kueleza kuwa anaguswa na ukomo wa uwezo wa Umoja wa Mataifa katika kutekeleza majukumu yake na mara kwa mara chombo hicho kinakosolewa.

Hata hivyo amesema licha ya mazingira hayo, bado Umoja wa Mataifa umesalia kuwa chombo ambamo kwacho mikataba muhimu na maazimio ya haki za binadamu hupitishwa na kuwa mwongozo wa misingi ya uhai wa binadamu.