Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi kuhamisha watu wengi zaidi duniani, hatua zachukuliwa

Mabadiliko ya tabianchi kuhamisha watu wengi zaidi duniani, hatua zachukuliwa

Mataifa 110 yameridhia ajenda ya ulinzi wa watu wanaolazimika kuvuka mipaka ya nchi yao kutokana na majanga na mabadiliko ya tabianchi.

Kupitishwa kwa ajenda hiyo kunafuatia mashauriano ya siku mbili ya mpango wa kimataifa wa Nansen, yaliyofanyika Geneva, Uswisi.

Ajenda hiyo inabainisha mazingira yanayokumba watu hao wakati huu ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limekuwa likipigia chepuo usaidizi kwa mataifa yanayopokea wakimbizi watokanao na majanga.

Volker Türk ambaye ni kamishna msaidizi, UNHCR amesema mafunzo yatokanayo na ukweli halisi wa mwelekeo wa ukimbizi hivi sasa ni fursa tosha ya kuzingatia athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga katika ukimbizi duniani kwenye mkataba mpya wa mabadiliko ya tabianchi utakaopitishwa Paris.

UNHCR inasema idadi kubwa ya wakimbizi Milioni 60 duniani hivi sasa wanaishi kwenye maeneo yanayokumbwa na mabadiliko ya tabianchi hivyo hali hiyo itazidi kuwa kichocheo cha watu kuhama makwao siku zijazo.