Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kirusi cha Ebola kinaweza kuishi katika shahawa kwa miezi tisa- WHO

Kirusi cha Ebola kinaweza kuishi katika shahawa kwa miezi tisa- WHO

Matokeo ya awali ya utafiti kuhusu uhai wa kirusi cha Ebola katika maji maji ya mwili yameonyesha kuwa baadhi ya wanaume bado hutoa sampuli za shahawa zinazopatikana kuwa na kirusi hicho zinapopimwa, hata baada ya miezi tisa tangu kuonyesha dalili za maambukizi.Amina Hassan anatuarifu zaidi.

(Taarifa ya Amina)

Ripoti hiyo iliyochapishwa leo katika jarida la masuala ya afya la New England, inatoa matokeo ya kwanza ya utafiti wa muda mrefu unaofanywa na Wizara za Afya na Ulinzi za Sierra Leone, Shirika la Afya Duniani, WHO na Vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia magonjwa.

Awamu ya kwanza ya utafiti huo imejikita katika kupima upatikanaji wa kirusi cha Ebola katika shahawa kwa sababu ya utafiti wa zamani ulioonyesha kuendelea kuishi kwa kirusi hicho katika maji maji hayo ya mwili.

Taarifa ya WHO imesema, kupata uelewa bora zaidi wa uhai wa kirusi cha Ebola katika shahawa ni muhimu katika kuwasaidia manusura kupona na kuendelea na maisha yao ya kawaida.