Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICTR imefanya kazi iliyotukuka: Jaji Joensen

ICTR imefanya kazi iliyotukuka: Jaji Joensen

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa leo limekutana kujadili ripoti ya mahakama ya kimataifa ya makosa ya kimbari dhidi ya watu wanaowajibika katika mauaji ya kimbari na uhalifu mwingine mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu yaliyotekelezwa dhidi ya raia wa Rwanda na nchi jirani kati ya Januari mosi hadi Desemba 31 mwaka 1994.

Akihutubia kikao hicho Rais wa ICRT, Jaji Vagn Joensen amesema mahakama ya kimataifa ya maujai ya Rwanda ICTR  ikiwa inaelekea kuhitimisa muda wake imefanya kazi muhimu licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa.

(SAUTI JOENSEN)

‘Licha ya changamoto sugu ya wafanyakazi, ICTR imepiga hatua kubwa katika kuandaa na kuhamisha nyaraka , kwenda katika mfumo wa kielektroniki , video na sauti  kwa ajili ya kutunza na usimamzi wa chombo hicho.’’

Kwa upande wake serikali ya Tanzania  ambayo imekuwa mwenyeji wa ICTR inayofikia ukomo wake, imesema uwepo wa mahakama hiyo  sio tu kuwa umekua funzo kwa falsafa ya sheria bali pia utafiti na mafunzo kwa vyuo vikuu.

Taarifa ya mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi inasema kuwa ICTR imefanya msaada wa mafunzo pia kwa elimu ya juu, mahakama za kimataifa na za kitaifa katika sheria ya kimataifa ya makosa ya jinai.