Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio 2242 la Baraza la Usalama lapigia chepuo wanawake na amani

Azimio 2242 la Baraza la Usalama lapigia chepuo wanawake na amani

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja limepitisha azimio namba 2242 ambalo pamoja na mambo mengine linasihi nchi wanachama kuweka mikakati na rasilimali zinazotakiwa kutekeleza ajenda ya wanawake, amani na usalama.

Azimio hilo lililowasilishwa na Uingereza, linazingatia uhusiano uliopo kati ya ushiriki wa dhati katika jitihada za kuzuia, kutatua na ujenzi baada ya mizozo.

Kwa mantiki hiyo azimio linataka pia nchi wanachama kuongeza usaidizi wa kifedha kwenye miradi ya kukwamua wanawake kiuchumi na kijamii baada ya mizozo, sambamba na kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa wa kimaendeleo hasa kwa wanawake.

Hata hivyo azimio hilo pia limeeleza masikitiko yake kuhusu kuendelea kwa tuhuma za ukatili wa kingono na unyanyasaji unaofanywa na walinda amani na vikosi visivyo vya Umoja wa Mataifa, likitaka uchunguzi ufanyike pamoja na nchi zinazochangia polisi kwa Umoja wa Mataifa kuwapatia watendaji wao mafunzo dhidi ya ukatili wa kingono kabla ya kutumwa kwenye maeneo ya kazi.