Skip to main content

Maarifa ya asili yanaokoa maisha UNESCO

Maarifa ya asili yanaokoa maisha UNESCO

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Irina Bukova amesema mchango wa maarifa ya kiasili katika kukabiliana na maafa kwa ajili ya ujasiri miongoni mwa wakazi wanaoishi katika mazingira magumu ulithibitika wakati wa tsunami iliyotokea katika Bahari ya Hindi mwaka 2004.

Amesema hayo katika sehemu ya ujumbe wake wa siku ya kupunguza majanga duniani hii leo ambayo ujumbe wake ni fursa ya kuzingatia umuhimu wa elimu na maarifa ya jadi katika kukabiliana na janga ya kiasili.

Bi. Bokova amesema mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa wa kupunguza maafa  uliofanyika  mwezi Machi 2015 mjini Sendai nchini Japan ulisisitiza hasa haja ya kuhakikisha elimu ya kiasili katika kukabili majanga inaeleweka kwa watu wengi zaidi kwa faida ya wote.

Kwa maantiki hiyo, Bokova amesema, tamko la Sendai linafanya kampeni ya ushirikiano mkubwa kati ya serikali Kuu, serikali za mitaa , jamii na watu wa asili katika uundaji na utekelezaji wa sera na viwango vya kuzuia maafa.