Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusiunge mkono harakati za wanawake kwa makofi tu bali vitendo: Lusenge

Tusiunge mkono harakati za wanawake kwa makofi tu bali vitendo: Lusenge

Harakati zinazongozwa na wanawake katika ujenzi wa amani na ulinzi duniani ni lazima ziungwe mkono ili ziweze kuwa endelevu na kuleta mabadiliko ya dhati, amesema Julienne Lusenge, Mkurugenzi wa mfuko wa wanawake huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakati akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani leo.

Bi. Lusenge amesema mfuko wao unahaha kuhakikisha wanakwamua kifikra na kiuchumi wahanga wa ukatili wa kingono nchini mwao na hatimaye wajumuike tena katika jamii kama wajumbe wa kuleta mabadiliko.

Hata hivyo amesema harakati hizo zinakumbwa na changamoto  ikiwemo wanaharakati wa haki za wanawake kutekwa na hata kubakwa na vikundi vilivyojihami hivyo akasema..

(Sauti ya Lusenge)

“Mafanikio ya juhudi hizi yanapaswa kuungwa mkono siyo kwa maneno tu na makofi, bali pia kwa hatua madhubuti na rasilimali. Umoja wa Mataifa unapaswa kubaini mbinu za kuhakikisha wanawake wanakuwa na majukumu rasmi katika ujenzi wa amani. Na ninaunga mkono tamko lililotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo.”

Zaidi ya wajumbe 110 wamejiorodhesha kuhutubia mjadala huo ambao ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 15 ya azimio namba 1325 la Baraza la Usalama kuhusu usawa wa kijinsia na amani na usalama duniani.