Siku ya kimataifa ya kupunguza maafa kauli mbiu, Maarifa kwa Maisha

Siku ya kimataifa ya kupunguza maafa kauli mbiu, Maarifa kwa Maisha

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema, maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya kimataifa ya kupunguza maafa yanaangazia nguvu ya maarifa ya jadi, na elimu ya kiasili katika kudhibiti hali hiyo. Taarifa kamili na Amina Hassan

(Taarifa ya Amina)

Katika ujumbe wake, Ban amepigia chepuo elimu ya kiasili, akisema maarifa ya jadi ni msingi wa taarifa kwa jamii nyingi kuishi kwa amani na mazingira yao, pamoja na kukabiliana na matukio ya usumbufu yatokanayo na mvurugiko wa hali ya hewa, kuongezeka kwa hali ya joto duniani na kuongezeka kiwango cha usawa wa bahari.

Ban ametolea mfano pia Cameroon, ambayo kupitia maarifa ya kijadi ya kuweka mbegu za mahindi na maharagwe kwenye beseni la maji kabla ya kupanda, husaidia wakulima kukabiliana na ukame.

Wakati huo huo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na udhibiti wa majanga, UNISDR, imetangaza jamii nane kuwa mabingwa wa kukabiliana majanga, ikiwemo jamii ya wakazi wa Nkolbikok, mjini Yaoundé, Cameroon. Jamii hiyo hupunguza hatari ya mafuriko na magonjwa kwa kushirikisha wanajamii wa kujitolea katika kuondoa taka kwenye mitaro na katika mfumo waliounda wa kuondoa taka.