Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Operesheni za amani ni kiini cha kazi ya UM duniani- Lykketoft

Operesheni za amani ni kiini cha kazi ya UM duniani- Lykketoft

Operesheni za amani ni kiini cha shughuli za Umoja wa Mataifa duniani, amesema Rais wa Baraza Kuu la Umoja huo, Mogens Lykketoft.

Bwana Lykketoft amesema hayo wakati wa mjadala wa Baraza Kuu kuhusu uimarishaji wa mfumo wa Umoja wa Mataifa, ambao umeangazia ripoti ya Katibu Mkuu namba A/70/357.

Rais huyo wa Baraza Kuu ameongeza kuwa operesheni hizo ni sehemu ya ubunifu mkubwa wa Umoja wa Mataifa tangu kuanzishwa kwake, ambao umeusaidia Umoja huo kutekeleza mamlaka yake na kuchangia pakubwa amani na usalama duniani.

Licha ya hayo, Bwana Lykketoft amesema kama chombo chochote kile, operesheni za amani zinahitaji kunolewa na kuboreshwa.

“Changamoto na matishio yanayoibuka kwa amani na usalama wa kimataifa yanafanya kuwepo haja ya Umoja wa Mataifa kuimarisha mchango wake, uwezo na utendaji kazi wake, hususan ule wa operesheni za amani. Mjadala wa leo unastahili na ni kwa wakati unaofaa.”

Amesema mzozo mkubwa wa wakimbizi na mizozo mingine ya kibinadamu na kiusalama inaonyesha jinsi mizozo ya sasa inavyotatnisha.

“Kwa muktadha wa hali hii halisi, ni lazima tufanyie marekebisho utendaji kazi na vyombo vyetu, jinsi tunavyoshughulikia masuala ya kisera na operesheni, na jinsi tunavyoshughulikia masuala ya bajeti na usimamizi.”