Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uwezo mkubwa wa chumi za Afrika haujatumiwa- Ban

Uwezo mkubwa wa chumi za Afrika haujatumiwa- Ban

Leo ikiwa ni wiki ya Afrika kwenye Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa Umoja huo, Ban Ki-moon, amesema uwezo mkubwa wa chumi za bara Afrika haujatumiwa, iwe ni wingi wa rasilmali au watu wake.

Ban amesema hayo wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wa kufungua wiki ya Afrika, akiongeza kuwa nchi za Afrika zinajikita katika kuboresha maisha kupitia elimu na afya bora, ajira zenye hadhi, mazingira safi na jamii jumuishi, zinazovumiliana, na zenye demokrasia.

Zinataka na zinastahili mustakhbali usio na mitutu ya bunduki kila mahali barani, na ambapo umaskini na njaa havina nafasi. Umoja wa Mataifa unaahidi kuunga mkono mpango wa miaka kumi wa kutekeleza Ajenda 2063, zikiwemo juhudi za jumuiya za kikanda za uchumi, zinapojitahidi kuungana zaidi.”

Aidha, Katibu Mkuu amesema ajenda ya pamoja ya 2030 kuhusu maendeleo endelevu inaunga mkono miungano ya kikanda katika kupanga, kutekeleza na kufanyia tathmini malengo ya maendeleo endelevu.